Saturday, 12 March 2016

Magufuli, Rais Vietnam wakubaliana mazito

RAIS wa Vietnam, Truong Tan Sang, ameondoka nchini jana baada ya kumaliza ziara yake ya siku nne. Pamoja na mambo mengine akiwa katika ziara yake nchini, kiongozi huyo amekubaliana na Rais John Magufuli, kuongeza mauzo baina ya nchi hizo mbili, kutoka Dola milioni 300 (Sh bilioni 630) za sasa hadi kufikia Dola bilioni moja (Sh trilioni 2.1) ifikapo mwaka 2020.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa majumuisho ya pamoja ya ziara ya Rais huyo nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga alisema ziara hiyo imekua na manufaa mengi na nchi hizi mbili zimekubaliana kuimarisha maendeleo na uhusiano.
Maeneo hayo ni pamoja na kukuza biashara baina ya Vietnam na Tanzania na kuhakikisha mauzo yanaongezeka kutoka dola milioni 300 kwa mwaka za sasa hadi kufika dola bilioni moja mwaka 2020.

Eneo jingine walilokubaliana ni Vietnam kuwekeza nchini hususan kwenye sekta ya kilimo cha mpunga, ufugaji wa samaki, uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao ya biashara na samaki pamoja na kufungua milango ya uhusiano wa kimataifa kwenye sekta ya mawasiliano ya simu kwa kualika wataalamu wa Vietnam kuja kufundisha Watanzania jinsi walivyoweza kuendelea kwenye sekta hiyo.
Balozi Mahiga pia alisema ziara hiyo imesisitiza kuimarisha uhusiano na kukuza diplomasia baina ya nchi hizo mbili na kuangalia jinsi ya kuwekeza kwa ubia katika sekta binafsi na serikali, lengo likiwa kupata faida pande zote. Kuhusu mazungumzo ya Rais Truong na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, wamekubaliana kuwepo na ushirikiano wa karibu baina ya mikoa ya Vietnam na Zanzibar ambayo ina mazingira yanayofanana.
Alisema ushirikiano huo uwe kwenye sekta ya utalii na ufugaji wa samaki, kwa kuwa Vietnam kuna mikoa yenye hali ya hewa na mandhari inayofanana na Zanzibar. Hata hivyo, Balozi Mahiga alisema kutokana na ziara hiyo, Rais wa Vietnam amemualika Rais Magufuli kutembelea nchi hiyo na mwaliko ambao Rais Magufuli ameukubali.
Aidha, Vietnam kupitia Waziri wake wa Habari, Nguyen Ban Son aliyeambatana na Waziri Mahiga, aliishukuru Tanzania kwa kuwapokea vizuri na kuomba kuendeleza uhusiano wao kimataifa pamoja na kuwaunga mkono kwenye harakati zao za kuwania nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2020 hadi 2021. Pia imeomba Tanzania kuunga mkono Vietnam kwenye harakati za kuwania nafasi katika Tume ya Sheria za Kimataifa (ILC), nafasi inayowania mwaka 2017 hadi mwaka 2021.
Wafanyabiashara Katika hatua nyingine, Rais Sang, ameahidi kuwapa ushirikiano wa kila aina wafanyabiashara wa Tanzania ili wanufaike na fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo nchini Vietnam. Alisema hayo alipokutana na uongozi wa wafanyabiashara wa Tanzania, mkutano ambao uliwahusisha pia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, Waziri Mwigulu, alisema mkutano huo ulikuwa wa manufaa makubwa na hasa katika makubaliano kuhusu uzalishaji wa sukari na mafuta ya kula, lakini pia maendeleo katika Sekta ya Kilimo na Uvuvi, huku akiongeza kuwa hayo ni maeneo ambayo yalipewa kipaumbele zaidi. “Tunalo soko kubwa na la uhakika la mafuta ya kula, tunaingiza kutoka nje ya nchi zaidi ya asilimia 80 ya mafuta yote ya kula tunayoyatumia hapa nchini,” alisema Mwigulu.
Alisema mataifa hayo mawili yamekubaliana kuingia ubia katika uwekezaji katika viwanda vya usindikaji, akisema wamekubaliana kuwa na muundo wa uhakika wa mawasiliano ili kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji. Kwa upande wake, Waziri Mwijage alisema Tanzania inayo mambo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam katika uzalishaji wa korosho na viwanda vya usindikaji wa zao hilo. Vietnam hivi sasa inazalisha tani 300,000 za korosho kwa mwaka.
Waziri Mwijage alisema katika mazungumzo hayo, pia mataifa hayo mawili yamekubaliana kuanzisha Kiwanda cha Tumbaku mkoani Tabora akiongeza kuwa nchi ya Vietnam inavyo viwanda 18 vya sigara, kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya nchi hiyo. Mazungumzo hayo yalimshirikisha pia Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzajia (TPSF), Dk Reginald Mengi na viongozi wengine wa taasisi za wafanyabiashara wa hapa nchini.
Rais Sang jana alihitimisha ziara ya kiserikali ya siku nne nchini. Akiwa nchini pia alitembelea Eneo Maalumu la Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), ambapo alisema atakaporejea nchini mwake atawahamasisha wafanyabiashara zaidi kuja kuwekeza nchini. Ujumbe wa Rais huyo wa Vietnam pamoja na kuwajumuisha mawaziri watano, pia uliwajumuisha wafanyabiashara 51, kutoka Vietnam ambao walitumia fursa hiyo kutengeneza mazingira ya uwekezaji nchini. Imeandikwa na Ikunda Erick na Oscar Mbuza.
SOURCE: HABARI LEO, GWIJI LA HABARI , 12 Machi 2016

No comments:

Post a Comment