Tuesday, 1 March 2016

BIASHARA NA UCHUMI YAWAASA WATANZANIA KUTONUNUA BIDHAA ZISIZO NA VIWANGO

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka Watanzania kuacha kununua bidhaa zisizo na viwango badala yake wabadili tabia kwa kununua bidhaa zinazokidhi viwango kwa matumizi mbalimbali.
Akizungumza katika kipindi maalumu na redio Capital Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile alisema kuwa kuwepo kwa wanunuzi wa bidhaa feki nchini kunachangia kuongezeka kwa bidhaa hizo sokoni.
Alisema iwapo Watanzania watabadilika na kuacha kununua bidhaa zisizo na viwango, uwepo wa bidhaa hizo utamalizika na kuwezesha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hizo kukosa masoko.

"Bado kuna tabia ya baadhi ya Watanzania wanaopenda kununua bidhaa zisizo na viwango kutokana na unafuu wake wa bei hali inayosababisha wafanyabiashara kuendelea kuingiza bidhaa zisizokuwa na viwango sokoni," alisema.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wote wanaozalisha bidhaa zisizokuwa na viwango ili kuwezesha masoko kuwa na bidhaa zilizokidhi viwango kwa ajili ya matumizi.
Aidha alisema TBS itahakikisha inaendelea kupambana na kuzikamata bidhaa zisizo na viwango ili kunusuru maisha ya watu na kuwataka wote wanaoingiza bidhaa hizo kuacha mara moja.
"Kupitia oparesheni zetu tutahakikisha tunazikamata bidhaa zisizo na viwango sokoni, na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuingiza bidhaa hizo kinyume na taratibu," alisema.

No comments:

Post a Comment