MAJAMBAZI WAUA, WAJERUHI KISHA WAPORA FUKO LA FEDHA
feb 2, 2016
MAJAMBAZI wawili wamevamia katika eneo la Kwa Aziz Ally na kupora kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana, kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Dar es Salaam jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Andrew Msata, alisema majambazi hao walivamia eneo hilo juzi saa moja usiku.
Alisema majambazi hao wakiwa wamepakizana katika usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda walivamia duka moja la jumla lililopo kwa Azizi Ally na baada ya uvamizi huo, walimkuta muuzaji aliyefahamika kwa jina la Saidi Msafiri (30), akihesabu fedha akiwa ameacha mlango mmoja wazi.
Alisema majambazi hao waliingia na kuchukua mfuko uliokuwa na fedha hizo. Kamanda, alisema kijana huyo alipojaribu kuwafuata kwa ajili ya kupambana nao, walifyatua risasi iliyompata tumboni na kupoteza fahamu kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke ambapo alipoteza maisha saa 9 usiku wa kuamkia jana.
Alisema kuwa baada ya majambazi hao kumpiga risasi, kupora fedha hizo walianza kukimbia kwa kutumia pikipiki hiyo ambayo namba zake hazikuweza kufahamika kutokana na giza na taa zake zilikuwa zimezimwa.
Alisema walipofika katika kituo cha daladala walianza kurusha risasi ovyo ili kuwatawanya wananchi ambapo miongoni mwao, wawili walijeruhiwa na kutibiwa katika Hospitali ya rufaa ya Temeke baada ya kupatiwa matibabu.
"Ni kweli tulipata taarifa na tulipofika eneo hilo tulikuta tayari tukio limeshatokea na majambazi wametokomea kupitia njia ya kwenda Mbagala, hivyo tulichukua watu waliojeruhiwa na kuwapeleka Temeke kwa matibabu ambapo mmoja alipigwa risasi tumboni na kuumia vibaya, amepoteza maisha na wengine wawili wamepewa ruhusa baada ya kupatiwa matibabu,"alisema.
"Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na kuwasiliana na mhusika ili kujua kiasi gani cha fedha kimeporwa na tutawasaka wahusika, kwani matukio kama haya huwa hayaanzi moja kwa moja ila wahusika huwa ni watu wa maeneo husika na wanachora ramani kabla ya kuvamia, lakini pia wananchi wanatakiwa waache tabia ya kukaa na fedha ndani badala yake wazipeleke benki kwa usalama zaidi,"aliongeza Kamanda Msata.
Naye Mariamu Juma mmoja wa masuhuda wa tukio hilo alisema kuwa kutokea kwa tukio hilo kumesababisha hasara hasa kwa wafanyabiashara kutokana na watu kukimbia ovyo kwa hofu na kuacha mali zao ili kuokoa maisha yao hivyo amelitaka jeshi la polisi kutilia mkazo suala hilo.
"Kwa kweli hali ni mbaya inatishia amani kwani walipofyatua risasi kila mtu hapa alichanganyikiwa baada ya kuona mtu ameuawa na wengine waliumia katika purukushani za kutaka kuwadhibiti majambazi ambao walianza kumimina risasi na kujeruhi watu,"alisema.
No comments:
Post a Comment