KAMPUNI SITA ZALIPA MIL. 200/- WASIFILISIWE
FRIDAY, FEBRUARY 26 2016
KAMPUNI ya Udalali ya Yono Auction Mart, imekusanya sh. milioni 200 kutoka kwa kampuni zinazodaiwa kukwepa kodi ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), baada ya kutorosha makontena na mizigo yao kwenye bandari kavu (ICD) ya Azam.
Fedha hizo zimelipwa na kampuni sita ambazo zimeitikia agizo la Serikali baada ya notisi ya muda waliopewa kulipa kuisha jana. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya Yono, Stanley Kevela, alisema kampuni 24 ziliisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 18 kwa kutorosha makontena bila kuyalipia ushuru.
"Kampuni yangu ilipewa kazi ya kuwafuatilia wadaiwa, hadi leo (jana), tumekusanya sh. milioni 200 kutoka kwa kampuni sita, pia tumekamata mali za kampuni mbili ambazo ni kontena tisa za bati pamoja na maghorofa," alisema Kevela.
Alisema kampuni 16 bado hazijatekeleza agizo la kulipa ushuru waliokwepa hivyo wanaendelea kuzifuatilia ili fedha hizo ziweze kupatikana na kutumika kwa maendeleo ya nchi.
Alizitaja kampuni zilizolipa fedha hizo kuwa ni Zulea All, Omary Hossein, Libas Fashion, Ally Handani, Zuleha Alli na Issa Salim.
Kampuni ambayo Yono imekamata kontena zao tisa za bati na nyingine 45 zipo bandarini ni Tifo Global Trading Co. Ltd na kampuni ya Tuff Tryes General Co.Ltd ambayo mali zake zimezuiwa na maghorofa vikisubiri kunadiwa na fedha zitakazopatikana zitapelekwa serikalini
No comments:
Post a Comment